top of page
Search
  • Mwamvua Mohamedy

Mwamvua Mohamedy - KIJANA NA AFYA BORA Fellow, Tabora.

Mwamvua Mohamedy, nimetokea Mkoa wa Tabora, Manispaa ya Tabora. Niliweza kupata fursa ya kujiunga kama mjumbe wa kujitolea katika Young & Alive Initiative kupitia mradi wa Kijana na Afya Bora. Kama kijana, niliona hii ni nafasi adhimu ya kujifunza stadi mbalimbali zinazohusiana na afya kwa vijana na kuboresha afya ya vijana pamoja na jamii kwa ujumla, ili kuleta mabadiliko katika jamii yangu, na uzoefu huu umenifundisha stadi muhimu za uongozi.


Fursa ya Kujifunza na Kujenga Uongozi katika Sekta ya Afya ya Uzazi kwa Vijana.

Nilituma maombi yangu na nikachaguliwa kushiriki kwenye mradi huu wa Kijana na Afya Bora pamoja na vijana wenzangu. Mafunzo tuliyopatiwa yaligusa maeneo mengi muhimu kama vile uongozi, ufuatiliaji wa huduma za afya ya uzazi jinsi zinavyotolewa, pamoja na jinsi ambavyo kijana anaweza kukusanya taarifa na kuwasiliana na makundi mbalimbali. Hii ilikuwa fursa kubwa kwangu kujifunza stadi nyingi zitakazonisaidia si tu kwenye mradi huu wa Kijana na Afya Bora, bali pia katika kujenga maendeleo ya jamii yangu kwenye sekta ya afya ya uzazi kwa vijana.

Pia, nikiwa kijana mwenye kiu ya kujifunza zaidi na kushiriki katika kuleta mabadiliko kwenye uongozi na afya ya uzazi kwa vijana, ningeomba mafunzo haya yafanyike ana kwa ana ili kumjengea kijana stadi mbalimbali kwa vitendo.


Changamoto katika jamii.

Kupitia mradi huu, nimeweza kushirikiana na wananchi, watoa huduma, pamoja na viongozi wa maeneo husika ili kujadili na kuleta mabadiliko. Tumeangazia changamoto mbalimbali zinazokabili jamii katika utoaji wa huduma za afya, hasa kwa vijana, ili huduma hizo ziwe rafiki kwao.


Vituo vya Afya vya Cheyo na Isevya, Manispaa ya Tabora.

Katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huu, niliweza kufanya kazi na vituo vya afya vya Cheyo na Isevya vilivyopo ndani ya Manispaa ya Tabora. Kazi yangu ilikuwa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa huduma za afya ya uzazi, hasa kwa vijana. Zoezi hili lilienda vizuri, ambapo tuliweza kufanya mahojiano na washiriki wote wakiwemo watoa huduma, wanajamii, na viongozi wa kata zote husika.


"Ninaamini kupitia mradi wa Kijana na Afya Bora tutaweza kuboresha afya ya uzazi kwa vijana na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii." - Mwamvua Moahmedy, Tabora.






6 views0 comments

Comments


bottom of page